Wajasiriamali Uyui wakopeshwa mil. 70/-

Category: Karibu katika Ujasiriamali

VIKUNDI zaidi ya 65 vya wajasiriamali wadogo kutoka katika kata zote wilayani Uyui mkoani Tabora, vimewezeshwa mikopo midogo ya zaidi ya Sh milioni 70 katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.


Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Hadija Makuwani katika kikao cha Baraza la Madiwani.

Makuwani alisema halmashauri yake imeanza kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli ya kuinua vikundi vya wajasiriamali, kwa kuhakikisha vikundi vyote vinawezeshwa mikopo midogo yenye riba nafuu ili kujikwamua kiuchumi.

Katika kutekeleza hilo, alisema tayari wametoa mikopo zaidi ya Sh milioni 70 kutoka katika mapato yake ya ndani na kuwezesha vikundi viwili viwili kutoka kila kata na katika robo ya mwisho ya mwaka huu, wanatarajia kutoa zaidi ya kiasi hicho ili kunufaisha vikundi vinne vinne katika kila kata, tofauti na awali.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Said Ntahondi alisema ili kufanikisha lengo hilo, atahakikisha kila fedha inayokusanywa, wanatenga mgawo wa asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa akinamama wajasiriamali na kila kikundi kitapata Sh milioni moja.

Ili kuongeza kasi na kuwezesha vikundi vingi zaidi, alisema wataweka uwiano mzuri wa utoaji mikopo hiyo ambapo watagawa kwa vikundi viwili vya vijana na vikundi viwili vya akinamama kutoka kila kata ili kuepusha malalamiko.

Chanzo: HABARILEO (http://www.habarileo.co.tz/index.php/biashara-na-uchumi/20559-wajasiriamali-uyui-wakopeshwa-mil-70)

Kuchapishwa: 30 Januari, 2017