Kubadili biashara si kosa, yatakiwa umakini

Category: Karibu katika Ujasiriamali

"INAWEZEKANA una sababu za msingi za kuacha biashara uliyoianzisha na kuidumisha kwa kipindi fulani. Kufanya hilo si kosa, ilimradi uamuzi wako usiwe wa kukurupuka, ili usikusukume kujuta baadaye."

Hivyo ndivyo unavyoeleza mtandao wa majibu www.answers.com, ukitoa maelezo mbalimbali kuhusu sababu za msingi zinazoweza kumfanya mfanyabiashara aachane na biashara moja na kuigeukia nyingine, bila kujali kuwa ya awali anayoiacha ilimgharimu muda na fedha nyingi za mtaji.

Kwa mujibu wa mtandao huo unaoendeshwa na wataalamu mbalimbali wa biashara, kuna wakati mfanyabiashara anapaswa kufanya uamuzi mgumu kunusuru maisha yake, kulinda utu wake, kudumisha uzalendo kwa nchi yake, kutokinzana na sheria za nchi anapofanya biashara, pamoja na kuepuka asiendelee kupata hasara zaidi, hasa ikiwa biashara husika 'haimlipi'.

Inaelezwa kuwa, kuna wakati mfanyabiashara anaruhusiwa kukubali hasara, lakini wakati huo hapaswi kufanywa kuwa mazoea. Ni lazima kukubali kwamba kuna mazingira mfanyabiashara analazimika kuingia gharama zaidi ili kukuza biashara yake, wakati mwingine kwa mtazamo wa haraka tunasema kwamba hiyo ni sehemu ya hasara, kwa sababu si mara zote gharama zinazotumika zinakuwa chini ya kinachopatikana, bali huwa juu maradufu ya kinachopatikana.

Wataalamu hao wa uchumi na biashara kupitia mtandao huo wanasema, inawezekana matumizi katika kuhakikisha kuwa biashara inaendelea kuwepo yanakuwa makubwa kuliko ukipatacho.

Hii huwezi kuihesabu kama faida, ingawa unapaswa kuikubali kwa malengo, hasa kama una uhakika kwamba baada ya muda fulani hali ya mapato itabadilika na kukuingizia faida kubwa itakayorudisha fedha zote ulizozitumia awali, kwa ajili ya kuijenga biashara yako.

Kwa sababu hiyo, wataalamu hao wanasema, dawa si kuiacha biashara yako na kuanzisha au kubaki kwenye nyingine, bali kuzitazama fursa zilizopo mbele ya safari ya biashara hiyo kuona endapo zitaweza kuziba mapengo ya fedha yaliyoachwa na matumizi makubwa wakati wa kuiendesha.

Hata hivyo, mtandao huo unasema kubadili biashara si kosa, bali kinacho hitajika ni umakini wa hali ya juu. Mtandao huo wa majibu unasisitiza kuwa, mfanyabiashara anapaswa kuangalia mambo muhumu matano kabla ya kuamua kubadili biashara.

Kwamba haiwezekani kuendelea kuwepo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo wateja kutohitaji bidhaa au huduma inayozalishwa katika biashara inayotakiwa kuachwa au kubadilishwa.

Katika hilo, inaelezwa kuwa itakuwa ni kupoteza muda kuendelea kung'ang'ana kuzalisha bidhaa ilhali wateja wote kwa wakati huo wamebadili mahitaji na kuchukua au kuhitaji bidhaa nyingine kama mbadala wa bidhaa yako.

Matokeo ya hatua hiyo ya wateja, ni kuifanya biashara yako ikose wanunuzi, hivyo kulazimika kuendelea kuwepo kwa hasara, hasa inapotokea kwamba mfanyabiashara husika hataki kusoma alama za nyakati, hashauriki au anafanya biashara ilimradi aonekane kuwa naye yumo.

Pia, inaelezwa kuwa, kuhama huko kwa wateja kutoka katika biashara yako na kufuata mbadala ni vyema kukafanyiwa utafiti kubaini endapo chanzo cha wateja kuihama biashara hiyo ni cha muda tu au ni cha kudumu.

"Ikiwa kukimbilia bidhaa mbadala hutokea kwa msimu mfupi tu, mfanyabiashara ana haki ya kutumia utaratibu au mbinu nyingine kupata mbadala wa bidhaa yake isiyotakiwa kwa kipindi husika, ili kuendelea 'kuwashikilia' wateja wasipotelee kwingine," ni ushauri unaotolewa kupitia mtandao huo.

Inafafanuliwa kwamba, kuwarejesha katika imani waliyokuwa nayo wateja kipindi cha mwanzo si jambo rahisi kama baadhi ya watu wanavyofikiria, hasa ikiwa wamekimbia kwa sababu wazijuao wenyewe, ni lazima maarifa sahihi yatumike kuhakikisha hawaikimbii biashara yako.

Mtandao huo unataja baadhi ya mbinu zinazoweza kutumika kuwafanya wateja wasiukimbilie mbadala wa bidhaa yako ulio katika duka jingine au ulio kwenye biashara ya mshindani wako kuwa ni pamoja na kuhakikisha unakwenda na wakati kwa kutangulia kuziandaa bidhaa mbadala ulizo na uhakika kwamba wakati msimu fulani ukifika, ni lazima wateja wako wataachana na bidhaa wazinunuazo na kuzikimbilia za mbadala.

Mfanyabiashara anaweza kuwashikilia wateja wake kwa kuwapa taarifa za mara kwa mara kuhusu mpango wa kuwaletea bidhaa wazitakazo pindi ufikapo msimu fulani ambao ni lazima wateja watahitaji bidhaa A na si bidhaa X inayozalishwa kila siku ili wasijipange kukimbilia kwingine.

Mtandao huo unasema kuwa taarifa ni silaha katika biashara na kwamba zikitumiwa ipasavyo zinaweza kuwa silaha bora za kumvusha mfanyabiashara kutoka katika hatua moja kwenda kwenye hatua nyingine yenye mafanikio zaidi.

Ili kuamua kuiacha biashara yako na kuhamia kwenye biashara nyingine, mfanyabiashara anashauriwa kuhakikisha anafanya utafiti wa kutosha wa wateja wa biashara anayotaka kuianzisha kama mbadala wa anayotaka kuiacha, ili kuepuka kurudia mambo yaliyomfanya afikirie kuiacha ya awali. Kwa maoni na maswali wasiliana na Mwandishi kupitia: Simu; 0752 779 090 au Baruapepe; namsp2000@ yahoo.com.

Chanzo: http://www.habarileo.co.tz/index.php/safu/23287-tuzungumze-biashara-kubadili-biashara-si-kosa-yatakiwa-umakini

Kuchapishwa: 07 Juni 2017 , Mwandishi: Namsembaeli Mduma