Watanzania wahamasishwa fursa bomba la mafuta

Category: Karibu katika Ujasiriamali

WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo katika Mradi wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Kabale Hoima, Uganda hadi Chongoleane Tanga, Tanzania kwa vile asilimia 80 ya bomba hilo litapita nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati anafungua kongamano la siku moja la kujadili ushiriki wa Watanzania katika mradi huo.

Huu ni moja ya miradi mikubwa inayotarajiwa kufanyika hapa nchini kwa thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5. Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 huku kilometa 1,149 zitapita nchini.

Ujenzi wa mradi huo utachukua miaka miwili mpaka mitatu na utapita katika vijiji 184, wilaya 24 na mikoa minane nchini ya Kagera, Tabora, Shinyanga, Geita, Dodoma, Singida, Manyara na Tanga na kutoa fursa nyingi katika maeneo hayo.

Waziri Mhagama alisema ili kufanikisha suala hilo, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati(Ewura) zinapaswa kuendelea kuelimisha wananchi kutumia fursa katika mradi huo. Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, alisema:

“Kongamano hili limelenga kuwawezesha Watanzania kufahamu fursa zilizopo kwenye mradi na jinsi watakavyoshiriki na kumiliki uchumi wa nchi kupitia mradi huu na mingine ya kitaifa.”

Alisema mradi huo unatarajiwa kutoa fursa za ajira 10,000 katika kipindi cha ujenzi na ajira 1,000 wakati wa uendeshaji. Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Louis Accaro, alisema:

“Tunataka wafanyabiashara wa Tanzania waainishwe ili kuona wanaofaa kuingia katika mradi huo, mfano zabuni zinapotangazwa lazima Watanzania wajulikane watakaoingia katika mradi ili wasije wakaachwa na kupewa watu wa nje.”

Chanzo: https://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/26506-watanzania-wahamasishwa-fursa-bomba-la-mafuta

Kuchapishwa: 25 Februari 2018  , Mwandishi: HABARILEO