Unaweza kuwa mjasiriamali !

Mambo mengi sana yanasemwa, yamesemwa na yataendelea kusemwa kuhusu ujasiriamali na wajasiriamali.  Wengi wamefanikiwa. Wamepita katika changamoto nyingi lakini hawakukata tamaa. Wengine, mafanikio yao yamebadilisha dunia kabisa na majina ya biashara zao ndio umekuwa wimbo katika midomo ya watu wengi.

Biashara za wajasiriamali , tena zilizofanikiwa, zimeanzishwa na wajasiriamali wa kila aina. Kila mtu ana hadithi yake na njia yake. Sio kwamba wote wamepita katika njia moja. Hapana! Wapo waliosoma sana, wapo ambao hawajasoma sana na wapo ambao wamesoma kidogo sana. Wengine hawakumaliza shule zao, bali waliishia katikati. Wengine walisoma kwa kiwango kikubwa kabisa. Lakini wote hawa, pasipo kutegemea walikotoka, ni wajasiriamali waliofanikiwa. Wote waliziona fursa, wakazichangamkia na sasa wamefanikiwa.

Baadhi ya wajasiriamali wamekuja na mawazo makubwa kabisa na ubunifu mwingi hata kuanzisha miradi, shughuli na biashara ambazo zimebadili jamii kabisa. Wapo ambao hugundua fursa baada kufanya utafiti wa kina katika mambo, wakitafakali kwa kina wachukue hatua gani sahihi na hata wakihusisha wataalamu mbalimbali katika kuwasaidia.

Lakini pia wapo wajasiriamali ambao wanapopata wazo la biashara , wanalirukia, wanakwenda nalo kama lilivyo na mambo mengine yatajijua mbele ya safari.

Mtu yeyote yule anaweza akafanikiwa katika biashara kama mjasiriamali. Hakuna sifa ya aina moja ambayo ndiyo kama kanuni inayotakiwa ili mtu afanikiwe kama mjasiriamali.

Je ni nini kinakuzuia usifanye ujasiriamali na kuwa mjasiriamali aliyefanikiwa? Endelea kutembelea tovuti ya mjasiriamali.co.tz maana unaweza kuwa mjasiriamali!