Wabunge wafundishwa uwekezaji

SERIKALI imewataka wabunge kuielewa dhana ya ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji (Local Content) ili wawe mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kiuchumi na uwekezaji nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama aliwaambia wabunge kuwa wao kama wawakilishi wa wananchi, wana nafasi kubwa ya kuwaelimisha kuhusu azma ya kuwawezesha Watanzania kuwa sehemu kubwa ya wamiliki wa uchumi.

“Mafunzo haya yanayotolewa kwenu yatasaidia kuleta mabadiliko chanya na jamii zitashirikishwa kikamilifu katika uwekezaji unaofanyika katika maeneo yao kupitia kwenu nyinyi wabunge,” alisema Jenista.

Akizungumza katika semina elekezi kwa Kamati za Bunge juu ya ushiriki wa wananchi katika uwekezaji, iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) mwishoni mwa wiki mjini hapa, Jenista alisema wakati umefika kwa Watanzania kuanza kunufaika kutokana na uwekezaji na hatimaye uchumi wa nchi kukua.

“Ni muhimu wananchi waliopo katika sehemu ambapo viwanda au miradi inaanzishwa kushirikishwa katika hatua za awali za uwekezaji au utekelezaji wa miradi,” alisema waziri huyo na kuongezea kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwazi na wananchi wajione ni sehemu ya maamuzi.

Alisema mafunzo hayo kwa kamati mbalimbali za Bunge pia yametoa nafasi kwa kwa wabunge kutambua majukumu ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo ndilo lenye dhamana ya kuratibu shughuli zote za uwezeshaji nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Dk John Jingu alisema uhusiano wa karibu kati ya wawekezaji na wananchi katika eneo ya mradi unatakiwa kuimarishwa ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji wa miradi katika maeneo yao.

“Changamoto kubwa ni ujuzi wa wananchi wetu katika uwekezaji na ushiriki wao,” alisema Dk Jingu na kuongeza kuwa baraza limejipanga katika kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu ya namna bora ya kushiriki katika uwekezaji na kukuza uchumi wao.

Mbunge wa Muheza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu alisema semina hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa wa wabunge kwani itawasidia kuwaelimisha wananchi juu ya ushiriki wao katika miradi inayofanyika katika maeneo yao.

“Tuna kila sababu za kuwaelimisha wananchi wetu juu ya kuongeza thamani ya bidhaa ili waweze kuendana na matakwa ya wawekezaji,” alisema Balozi Adadi na kuongezea kuwa sheria zinawalinde wazawa katika ushiriki wao katika uwekezaji.

Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka alisema ni vyema baraza pamoja na wadau wengine watathmini mambo yaliyofanyika na yanayotarajia kufanya ili watu wote wawe lugha moja juu ya ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.

 Chanzo (HABARILEO) : http://www.habarileo.co.tz/index.php/biashara-na-uchumi/20578-wabunge-wafundishwa-uwekezaji

Mwandishi: Magnus Mahenge , 31 Januari 2017