Dk Yonazi ataka wananchi waelimishwe fursa zilizopo

MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk Jim Yonazi ametaka wananchi wahabarishwe juu ya fursa zilizopo ili kufikia uchumi wa viwanda.

Dk Yonazi alisema hayo kwenye Ukumbi wa Kambarage katika Jengo la Hazina mjini hapa wakati akizungumza kwenye Kongamano la Pili la Uwezeshaji lililoandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Alisema wananchi wataweza kushiriki katika uchumi wa viwanda kama watahabarishwa kuhusu fursa mbalimbali zilizopo nchini hivyo kuwa na mchango mkubwa. “Ukiangalia Malengo ya Maendeleo ya Milenia ni lazima uwe na jamiii ambayo imehabaribishwa.

Sasa hapa ndipo mchango wetu sisi wengine unaingia, sekta nyingine binafsi ya serikali, lakini kwa upande wa habari,” alisema Dk Yonazi, ambaye TSN inayomiliki magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo ilidhamini kongamano hilo la pili kufanyika nchini.

Alisema ni lazima nchi iwe imehabarishwa na ili ihabarishwe, lazima kuwa na mambo kadhaa yanayofanyika katika sera, fursa na mifumo ya udhibiti, ili jamii kwa ujumla wake ifahamu mambo mbalimbali.

Alifafanua kwamba TSN iko tayari kushirikiana na serikali na sekta binafsi katika kuhabarisha wananchi kuhusu fursa hizo za kiuchumi kuelekea uchumi wa viwanda. Alielezea kuhusu kampuni hiyo inavyoendesha Jukwaa la Biashara ambalo tayari limefanyika kwa mafanikio makubwa katika mikoa miwili ya Simiyu na Mwanza.

Alisema lazima sekta binafsi iibue matatizo ambayo yanageuka kuwa fursa zitakazoiwezesha sekta hiyo kuibua kitu kingine; ubunifu na hivyo kuleta utatuzi wa matatizo na baadaye kuja na mifumo. Katika udhibiti, alisema ndipo ambapo serikali huingia kwa sababu ni muhimu kuwa na udhibiti ili kinachopatikana kigawanywe kwa wote. Alisema serikali wajibu wake ni kwa kila mtu.

“Kazi ya serikali ni kuhakikisha utajiri wa habari, fedha, ujuzi, utajiri wa nchi, na kisera, unakwenda kwa watu wote. Na naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano imeona hili kwa kusaidia wananchi kiuchumi.

“Ukimnyima mwananchi fursa anaishia kuwa maskini, ukimnyima utajiri wa ujuzi, utajiri wa fedha, utajiri wa mahusiano na utajiri wa amani, unamtengenezea umaskini. Hapa ndipo serikali inapoingia ili kuhakikisha kuwa uchumi huu unaendeshwa fairly (kwa haki),” alieleza Dk Yonazi.

Chanzo: http://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/23394-dk-yonazi-ataka-wananchi-waelimishwe-fursa-zilizopo

Kuchapishwa: 12 Juni 2017 , Mwandishi: HABARILEO