'Watanzania changamkieni fursa bomba la mafuta'

KATIBU wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa amewahimiza wafanyabiashara nchini, kujiunga katika vikundi ili kupata sifa za kuzitumia vema fursa katika mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga..

Ameyasema hayo Dar es Salaam katika kongamano la siku moja kujadili ushiriki wa Watanzania katika mradi wa ujenzi wa bomba hilo.

Ujenzi utachukua miaka miwili mpaka ukipita katika vijiji 184, wilaya 24 na mikoa minane na kutoa fursa nyingi katika maeneo hayo huku ukitoa ajira 10,000 katika kipindi cha ujenzi na ajira 1,000 wakati wa uendeshaji.

Kwa mujibu wa Issa, kongamano hilo lililenga kuwawezesha Watanzania kufahamu fursa zilizo katika mradi unaopita katika mikoa ya Kagera, Tabora, Shinyanga, Geita, Dodoma, Singida, Manyara na Tanga.

Isaa alitoa mwito kwa wafanyabiashara wanaotaka kutumia fursa hizo kujiandikisha kwenye kanzidata ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), huku wananchi wengine wakijiandikisha katika taasisi inayoshughulikia masuala ya ajira (TAESA) au Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Kazi na Ajira. Mkurugenzi wa Gesi Asilia wa Ewura, Charles Omujuni, alisema:

“Tumejipanga kutoa leseni kwa kampuni itakayoundwa kusimamia mradi huu.” Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alinukuliwa akiwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa hizo.

Chanzo: https://www.habarileo.co.tz/index.php/biashara-na-uchumi/26558-watanzania-changamkieni-fursa-bomba-la-mafuta

Kuchapishwa: 27 Februari 2018  , Mwandishi: HABARILEO