‘Wapeni wananchi elimu ya mikopo, msikae ofisini’

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amewataka watendaji wakuu na wafanyakazi wa idara za mikopo za benki, taasisi za fedha na mifuko ya kijamii kote nchini, kuacha kukaa ofisini na badala yake kwenda vijiji kutoa elimu kwa wananchi juu ya fursa za kukopa ili wajiinue kiuchumi.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amewataka watendaji wakuu na wafanyakazi wa idara za mikopo za benki, taasisi za fedha na mifuko ya kijamii kote nchini, kuacha kukaa ofisini na badala yake kwenda vijiji kutoa elimu kwa wananchi juu ya fursa za kukopa ili wajiinue kiuchumi.

Dk Mpango alisema hayo wakati akifungua mkutano wa 18 wa Wakuu wa Benki na Taasisi za Fedha nchini, uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 300 wa ndani na nje ya nchi.

Alisema Watanzania wengi hasa vijijini hawana elimu wala uzoefu wa kukopa benki na kwenye taasisi nyingine za fedha, hivyo wanahitaji kupata elimu ya kutosha ya namna ya kukopa, lakini wanashindwa kufanya hivyo kwa kuwa hawana elimu.

Aliwataka watendaji katika taasisi za fedha kwenda vijijini kutoa elimu hiyo. Dk Mpango alisema nchi ina fursa nyingi na jiografia yake inaruhusu, hivyo viongozi wa taasisi za fedha na wataalamu katika siku mbili za mkutano huo kujipanga vizuri na kuibua mkakati utakaoweza kusaidia Watanzania wanufaike na fursa hizo.

Alisema katika maazimio yaliyopita ya mkutano, waliazimia kuongeza mikopo katika sekta ya kilimo, lakini makubaliano na maazimio hayo hayakufanyika wala kutekelezwa.

Kutokana na hilo, aliwataka wataalamu kuhakikisha yanatekelezwa ili kuinua uchumi wa nchi, kwani kilimo ni uti wa mgongo wa nchi.

Akizungumzia ugumu wa maisha unaolalamikiwa na baadhi ya watu wanaoeleza kuwa uchumi umekuwa mgumu, Waziri wa Fedha alisema si kweli kwa sababu tafiti zote za ndani na nje ya nchi zimekuwa zikitoa taarifa kuwa uchumi wa nchi unakua siku hadi siku.

Dk Mpango alisema wanaosema kuwa hali ya kifedha ni ngumu ni wale waliozoea ‘kupiga madili’ na kupata fedha nyingi kwa njia zisizo halali, jambo ambalo kwa sasa halipo kutokana na ukweli kuwa mianya karibu yote waliyokuwa wakiitumia kujaza fedha mifukoni mwao imezibwa.

Aliwataka Watanzania kuacha kulalamika na badala yake kufanya kazi kwa bidii na kupata fedha kwa njia halali.

Gavana wa Benki Kuu Tanzania, Profesa Benno Ndulu alizitaka benki, taasisi za fedha na mifuko ya jamii nchini kutoa mikopo kwa wingi na kwa riba nafuu ili wakopeshwaji ambao ni wakulima na wafanyabiashara wafanye shughuli hiyo kwa uhakika zaidi.

Chanzo (HABARILEO) :  http://www.habarileo.co.tz/index.php/biashara-na-uchumi/17953-wapeni-wananchi-elimu-ya-mikopo-msikae-ofisini

Mwandishi: John Mhala, Arusha , kuchapishwa 24 Novemba 2016